Thursday, February 2, 2012

Bunge laingilia mgomo

HATIMAYE Bunge limeingilia kati mgomo wa madaktari kwa kuitaka Serikali kulitolea tamko tatizo hilo leo bungeni, vinginevyo ratiba ya shughuli zake itavurugwa na baadhi ya wabunge wanaotaka suala hilo lijadiliwe.

Naibu Spika,  Job Ndugai alitoa agizo hilo jana wakati anaahirisha kikao cha mchana akisema: "Serikali haina budi kujipanga ili leo itoe kauli kuhusu suala hilo."

Ndugai alisema Misri kulikuwa kuna mchezo wa mpira, kukatokea fujo uwanjani na kusababisha vifo vya watu mbalimbali, Bunge lilikuwa likizo lakini limeitwa kwa dharura kujadili suala hilo.

Ndugai aliongeza; “Hapa nyumbani (Tanzania) kuna mgomo wa madaktari unaendelea, asubuhi wamesimama wabunge kuleta hoja ya dharura lakini haikuungwa mkono. Litakuwa jambo lisiloeleweka kama kesho (leo) kauli ya Serikali haitatoka, wakisimama wabunge ratiba yetu inaweza kutibuka.”

Awali, baada ya kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndungulile (CCM), alisimama kwa kutumia kanuni namba 47 (i) na kutaka Bunge lijadili mgomo wa madaktari unaoendelea nchini.

Hoja hiyo ambayo baadaye iliungwa mkono na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), lakini ilitupwa na Ndugai kwa madai kuwa haikuungwa mkono na wabunge wengine.

Viongozi wa dini

Viongozi wa dini wa Kikristo na Kiislam jana walianza juhudi za kusaka suluhu ya mgogoro huo katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi.

Viongozi wa dini walioshiriki kikao hicho ni mkuu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya hospitali hiyo, Askofu wa KKKT Dayosisi ya kaskazini Dk Martin Shao, Katibu wa Baraza la Waislamu (Bakwata) Mkoa wa Kilimanjaro, Rashid Malya, Msaidizi wa askofu jimbo katoliki Deodatus Matika na Mkuu wa wilaya ya Moshi Musa Samizi aliyemwakilisha Mkuu wa mkoa huo, Leonidas Gama.

Akizungumzia majadiliano Dk Alex Malasusa alisema:” Ulikuwa mkutano wa kawaida uliokuwa na lengo la kuhimiza na kushauriana juu ya madai ya madktari na tumewakumbusha wajibu wao na kuzingatia viapo vyao”, alisema.

Katibu  wa Bakwata, Shehe Mallya aliungana na viongozi wengine kutoa wito kwa madaktari waliogoma kurudi kuwahudumia wagonjwa ambo kwa sasa wanaendelea kukosa huduma mbalimbali za afya.

Muhimbili
Madaktari bingwa  katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), wameungana na kamati ya madaktari inayosimamia mgomo na kuitaka Serikali kujibu hoja za zilizowasilisha kwake haraka ili kumaliza tatizo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha pamoja kati ya kamati hiyo na viongozi wa jumuiya ya madaktari, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Dk Stephen Ulimboka alisema wamekubaliana kuwa masuala yote yanayohusu mgogoro huo na maslahi ya madaktari yafanywe na kamati iliyoteuliwa na madaktari
 imenukuliwa kutoka http://www.mwananchi.co.tz/habari/4-habari-za-kitaifa/19911-bunge-laingilia-mgomo-wa-madaktari